-->


Anaandika Abdullatif Yunus, Michuzi TV.
Mkuu wa wilaya ya Muleba, Mhandisi Richard Ruyango, amekabidhiwa jengo la Mdhibiti na Mkaguzi wa shule, na Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Muleba Ndg. Emmanuel Sherembi, kisha alilizindua na kulikabidhi kwa Mkaguzi na Mdhibiti Ubora wa Elimu wilaya ya Muleba Ndg. Josephat M. Joseph kwa ajili ya kuanza kutumika.

"Tangu awamu ya tano iingie madarakani inapambana kuboresha miundombinu na hali ya elimu ambapo ilianza na elimu bure kwa wanafunzi wa shule za msingi na sekondari, malipo kwa waratibu elimu na wakuu wa shule kwa ajili ya kuwarahisishia kwenye majukumu yao ya kila siku na sasa imeamua kujenga ofisi za Wadhibiti Ubora wa Elimu kwa kila wilaya ili wawe na ofisi nzuri za kufanyia kazi na sekta ya elimu izidi kufanya vizuri", alieleza Mhandisi Richard Ruyango.

Aidha, amepongeza juu ya ubora wa jengo kutokana na usimamizi wa karibu wa wataalam na matumizi mazuri ya fedha hadi kupelekea kubaki na kiasi cha Tsh. 13,934,379.73

Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia ilitoa kiasi cha Tsh. 152,032,650.00 kwa ajili ya ujenzi wa jengo hilo ambapo kiasi cha fedha kilichotumika ni  Tsh. 138, 098,270.27 na hivyo kubaki na kiasi cha Tsh. 13,934,379.73.

Katika hafla hii iliyofanyika leo tarehe 01.10.2019 pia amehudhuria Mwenyekiti wa Halmashauri ya wilaya ya Muleba, Mheshimiwa Kamugisha Chrisant, Mkurugenzi Mtendaji, Ndg. Emmanuel Sherembi, Kamati ya Ulinzi na Usalama na Wakuu wa Idara wa Halmashauri ya wilaya ya Muleba.

Hayo yanajili siku moja baada ya Mkuu wa Mkoa Kagera Brig. Jen. Marco Gaguti kuzindua rasmi majengo hayo kwa Wilaya zote za Mkoa wa Kagera ambapo zoezi la uzinduzi huo likifanyika Wilayani Karagwe ambapo wilaya hiyo Imebaki na Shilingi milioni saba chenji, katika bajeti ya pesa yote ya mradi.