-->

Mamlaka ya Dawa na Vifaa tiba (TMDA) inaendesha mafunzo maalum ya siku tano kwa wakaguzi  wa dawa wa Halmashauri za Mkoa wa Pwani yanayoendana na kuzingatia maadili, uweledi pamoja na uelewa wa kanuni na sheria ikiwemo suala la usimamizi wa  dawa zenye asili ya kulevya  ili kuhakikisha kuwa zinatumika  kwa matumizi yanayotarajiwa na si vinginevyo katika kulinda Afya za Jamii.

Awali akifungua mafunzo hayo yanayoendelea katika ukumbi wa Baraza la Wauguzi na Ukunga (TNMC) Kibaha Mkoani Pwani,   mgeni rasmi ambaye ni Mganga Mkuu wa Mkoa wa Pwani, Dkt. Gunini Kamba amewapongeza TMDA kwa hatua hiyo kwani imekuja kipindi muafaka kwa watalaam hao  kwani mkoa huo umejipanga kuwa kitovu cha viwanda vya dawa na vifaa tiba pamoja na viwanda vingine.


“Mkoa wa Pwani unaendelea kuhamasisha uanzishwaji wa viwanda vikiwemo vya kawaida na vya dawa. Wataalam wetu wekitoka hapa watakuwa msaada na kuongeza chachu ya kuwezesha ukaguzi na ufuatiliaji  na kutimiza wajibu wao.
"Pia naamini  mtajifunza mbinu za kukabiliana na dawa na vifaa tiba duni na bandia  na utoaji wa taarifa kuhusiana na madhara yatokanayo na madhara ya matumizi ya bidhaa za dawa.” Alieleza Dk.Kamba


Aidha, Dk. Kamba alisema kuwa, katika dhana ya viwanda, Mkoa wa Pwani umekuwa mstari wa mbele katika kuvutia wawekezaji wa viwanda hususani vya dawa na vifaa tiba.
“Mpaka sasa tuna viwanda sita ambavyo vimeanza kujengwa tangu serikali ya awamu ya tano imeingia madarakani. Viwanda hivi vitaongeza ajira kwa wananchi wa Mkoa wetu lakini pia kuzuia fedha zetu kwenda nje kufuata dawa ..naamini tutapiga hatua na tutaendelea kutimiza wajibu wetu” alimalizia Dk. Gunini.


Kwa upande wake Meneja wa Kanda ya Mashariki  wa TMDA,  Adonis Bitegeko ameeleza kuwa mafunzo hayo yatalenga kwenye utendaji sahihi na uelewa kama taratibu za Mamlaka zinavyolenga.


“Katika uzoefu wa kufanya ukaguzi imeonekana mapungufu kwa baadhi ya wakaguzi wetu hivyo katika mafunzo haya tutajitahidi wakaguzi waelewe na watambue namna ya kubaini dawa duni na  bandia pia washiriki watapatiwa mafunzo ya kuzingatia miongozo katika ukaguzi wa viwanda vinavyozalisha na dawa na vifaatiba ili kuwezesha uzalishaji wa dawa bora, salama na fanisi alisema Adonis Bitegeko.


Nae Mratibu wa ofisi za Kanda  na Halmashauri za TMDA, Dkt. Henry Irunde akisoma taarifa ya utangulizi ya mafunzo hayo, akimwakilisha Mkurugenzi wa TMDA, alibainisha kuwa, jukumu kubwa la watalaam hao kuhakikisha wanazingatia maadili ya kazi zao katika kulinda afya ya jamii kwa kudhibiti ubora, usalama na ufanisi katika dawa na vifaa tiba nchini.


“ufanisi wa dawa na vifaa tiba ni jambo muhimu sana  katika kuboresha afya ya jamii. Hadi sasa zaidi ya asilimia 80 ya dawa zinazotumika nchini zinatoka nje ya nchi. 

Pamoja na kwamba udhibiti katika vituo vya forodha na katika soko umeimarishwa, bado kuna changamoto ya uwepo wa dawa duni, bandia na ambazo hazijasajiliwa hivyo dawa hizi hazina  budi kufuatiliwa na kuondolewa  kwenye soko hivyo mafunzo haya tutapata wakaguzi wenye weledi katika kutambua dawa na vifaa tiba visivyofaa kwa matumizi pamoja na kuhamasisha uwekezaji na ukuaji wa viwanda vya dawa na vifaa tiba hapa nchini” Alisema Dkt. Irunde.

Mafunzo hayo ya siku tano  yaliyoanza Septemba 30, yanatarajiwa kufikia tamati Oktoba 4, mwaka huu huku yakizingatia masuala muhimu  kwa wakaguzi hao ni pamoja na kuwakumbusha maadili na taratibu za kazi katika kutumiza majukumu yao. Pia uwelewa wa kanuni za uzalishaji pamoja na miongozo ya usambazaji wa dawa, vifaa tiba na vitendanishi nchini.
 Mganga Mkuu wa Mkoa wa Pwani, Dkt. Gunini Kamba akizungumza na waandishi wa habari baada ya kufungua mafunzo maalum ya siku tano kwa wakaguzi  wa dawa wa Halmashauri za Mkoa wa Pwani.
 Meneja wa Kanda ya Mashariki  wa TMDA,  Adonis Bitegeko akizungumza na waandishi wa habari  wakati wa ufunguzi wa mafunzo maalum ya siku tano kwa wakaguzi  wa dawa wa Halmashauri za Mkoa wa Pwani.
 Meneja wa Kanda ya Mashariki  wa TMDA,  Adonis Bitegeko(kulia)akisisitiza jamabo kwa Washiriki wa  mafunzo maalum ya siku tano kwa wakaguzi  wa dawa wa Halmashauri za Mkoa wa Pwani.(Picha na Emmanuel Massaka wa Michuzi Tv)
Washiriki wa Mafunzo  wakimsikiliza Mganga Mkuu wa Mkoa wa Pwani, Dkt. Gunini Kamba.