-->

 Na Karama Kenyunko,Michuzi TV

WAFANYAKAZI tisa wa Shirika la Taifa la Hifadhi ya Jamii (NSSF), akiwemo  Kaimu Mkurugenzi wa Fedha Jamila Vulu wamefikishwa Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, wakikabiliwa na kesi ya uhujumu uchumi yenye  mashitaka matano yakiwemo ya kughushi na kutakatisha fedha wa zaidi ya Sh. bilioni mbili.

Mbali na Vulu, washitakiwa wengine ni Kaimu Mkurugenzi wa Rasilimali Watu, Tikyeba Alphonce, Mwandishi wa hundi, Abdulrahaman Njozi, Meneja Uhakiki, Amir Kapera, Mhasibu anayehusika na maridhiano, James Oigo, Hellen Peter Mhasibu Mkuu,  Ivonne Kimaro Mhasibu Mwandamizi anayeshughulikia matumizi, Restiana Lukwaro Mhasibu dawati la Uchunguzi na Dominic Mbwete Mhasibu.

Akisoma hati ya mashtaka, Wakili wa Serikali Mwandamizi, Wankyo Simon amedai mbele ya Hakimu Mkazi Mwandamizi Mfawidhi, Kelvin Mhina kuwa kati ya Julai Mosi, 2016 na Septemba 4,mwaka 2017 maeneo mbalimbali ya jiji la Dar es Salaam, washitakiwa walikula njama ya kutenda kosa la kughushi na utakatishaji fedha haramu.

Imedaiwa, kati ya Julai Mosi mwaka 2016 na Septemba 4,mwaka 2017 katika Ofisi za NSSF Makao Makuu zilizopo katika Wilaya ya Ilala, jijini Dar es Salaam, washtakiwa Njozi na Kapera kwa nia ya kulaghai walighushi hundi 47 za benki ya CRDB
Kwa jina la NSSF yenye fedha Sh 2,130,211,437 huku wakionesha kuwa hundi hizo ni halali na na zimetolewa na bodi ya wadhamini ya shirika hilo.

Imedaiwa kuwa, siku na mahali hapo washitakiwa wakiwa watumishi wa umma na waajiriwa kwa vyeo hivyo, waliiba Sh. 2,130,211,437 mali ya bodi ya wadhamini ya NSSF

Aidha katika shtaka la nne la kusababisha hasara, inadaiwa washitakiwa wote hao wakiwa watumishi wa umma na waajiriwa wa NSSF, walisababishia shirika hilo hasara ya Sh. 2,130,211,437 kwa kushindwa kutekeleza majukumu yao.

Kati ya Julai Mosi mwaka 2016 na Septemba 4, mwaka 2017 katika Ofisi za NSSF Makao Makuu wilayani Ilala, Dar es Salaam, washtakiwa wote walijihusisha na miamala mbalimbali huku wakijua fedha hizo ni mazalia ya makosa tangulizi ya kughushi na wizi.

Hata hivyo washtakiwa hawakuruhusiwa kujibu chochote mahakamani hapo kwa sababu mahakama hiyo haina mamlaka ya kusikiliza kesi za uhujumu uchumi.

Kwa mujibu wa upande wa mashtaka upelelezi wa shauri hilo bado haujakamilika 

Wakili wa utetezi, Alex Mushumbuzi aliuomba upande wa mashitaka kuhakikisha wanaongeza spidi katika upelelezi kwa sababu mpaka washitakiwa wanaletwa mahakamani wanaamini kuna mchakato ulianza kufanyika.

Kesi hiyo imeahirishwa  hadi Oktoba 15 mwaka huu kwa ajili ya kutajwa na washitakiwa wamerudishwa rumande.

WAFANYAKAZI tisa wa Shirika la Taifa la Hifadhi ya Jamii (NSSF), akiwemo Kaimu Mkurugenzi wa Fedha, Jamila Vulu wamefikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, wakikabiliwa na kesi ya uhujumu uchumi yenye mashitaka matano yakiwemo ya kughushi na kutakatisha fedha wa zaidi ya Sh. bilioni mbili.