-->

Na Teresia Mhagama, Dodoma
Waziri wa Nishati, Dkt Medard Kalemani, ameagiza kuwa wakandarasi wa umeme vijijini wenye mikataba wahakikishe kuwa wanamaliza kazi za usambazaji umeme vijijini ifikapo tarehe 31 Disemba mwaka huu.

Dkt Medard Kalemani aliyasema hayo hivi karibuni wakati wa kikao chake na Wafanyakazi, Menejimenti na Bodi ya Wakala wa Nishati Vijijini (REA).

 Kikao hicho kilifanyika jijini Dodoma na kuhudhuriwa na Viongozi mbalimbali wa Wizara ya Nishati, akiwemo Kaimu Katibu Mkuu, Raphael Nombo, Kamishna wa Umeme na Nishati Jadidifu, Mhandisi Leonard Masanja na Kamishna Msaidizi wa Maendeleo ya Nishati, Mhandisi Juma Mkobya.

“Kila mtumishi anayehusika na suala hili, ahakikishe kuwa anasimamia ipasavyo kazi yake ili lengo litimie, iwe ni mtu wa fedha, mhandisi, mtu wa manunuzi, lengo ni kupeleka umeme vijijini kwa muda uliopangwa na kwa ufanisi.” Alisema Dkt Kalemani.

 Kufuatia agizo hilo, Dkt Kalemani aliwataka watumishi wa REA kuanza maandalizi ya utekelezaji wa mradi wa umeme vijijini wa Awamu ya Tatu mzunguko wa pili (REA III, Round II) ili ifikapo tarehe 31, Januari 2020, utekelezaji wake uanze.

  “ Bado kuna muda wa kutosha wa maandalizi, hivyo kama kuna sheria, kanuni na taratibu zinazopaswa kufuatwa, zizingatiwe na masuala yote yafanyike ndani ya muda, ili utekelezaji uanze, lengo letu sote ni kufikisha umeme kwenye vijiji vyote ifikapo mwaka 2021.” Alisema Dkt Kalemani.

Waziri wa Nishati pia aliagiza kuwa, Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) na REA washirikiane katika kusimamia utekelezaji wa miradi ya umeme vijijini na kuwachukulia hatua wakandarasi wazembe.

 Aidha alitoa agizo kuwa, wakandarasi wote wa umeme vijijini mara wanapomaliza kazi waliyopangiwa na Serikali, wanapaswa kufanya makabidhiano na TANESCO au REA badala ya kuondoka kiholela katika maeneo waliyopangiwa kusambaza umeme ili kujirisha na masuala mbalimbali ikiwemo kama kazi husika imezingatia ubora na wigo.

 Vilevile, aliendelea kusisitiza kuhusu suala la wasimamizi wa miradi ya umeme vijijini, kufuatilia kwa karibu kazi zinazoendelea za usambazaji umeme vijijini badala ya kutumia muda mwingi kuwa maofisini.

Waziri wa Nishati na Kaimu Katibu Mkuu, pia walizungumza na watumishi wa REA kuhusu masuala kiutumishi ambayo yatapelekea utatuzi wa changamoto mbalimbali na kuongeza morali ya kazi kwa watumishi hao.

Kwa upande wake, Kamishna wa Umeme na Nishati Jadidifu, Mhandisi Leonard Masanja alisisitiza kuhusu suala la kufuata haki na sheria wakati wa mchakato wa kupata wakandarasi wa umeme vijijini ili kuepuka migogoro itakayochelewesha utekelezaji wa miradi.

Aidha, alisema kuwa agizo la Waziri, kuhusu wasimamizi wa miradi ya umeme vijijini kwenda katika maeneo ya kazi ili kusimamia kazi hizo kwa karibu halina budi kutekelezwa kwani ni jukumu la Taasisi kusimamia miradi hiyo.

Kwa upande wake, Kaimu Mwenyekiti wa Bodi ya REA, Dkt Andrew Komba alimshukuru Waziri wa Nishati kwa kufanya kikao na Bodi, Menejimenti na Wafanyakazi wa REA na kueleza kuwa vikao vya aina hiyo, vinasaidia kutoa mwelekeo wa Serikali inakotaka kwenda na kufanya utatuzi wa changamoto mbalimbali.

Dkt Komba pamoja kueleza masuala mbalimbali ambayo yamefanyiwa kazi na Bodi hiyo ili kuboresha masuala la kiutumishi na kazi za usambazaji umeme vijijini, aliahidi kuwa Bodi hiyo itayazingatia maagizo yaliyotolewa na Waziri wa Nishati.
 Waziri wa Nishati, Dkt Medard Kalemani akizungumza katika  kikao chake na Wafanyakazi, Menejimenti na Bodi ya Wakala wa Nishati Vijijini (REA). Wengine katika picha Kaimu Katibu Mkuu, Wizara ya Nishati, Raphael Nombo (kulia kwa Waziri), Kamishna wa Umeme na Nishati Jadidifu, Mhandisi Leonard Masanja (wa kwanza kushoto), Mjumbe wa Bodi ya REA, Dailin Mgweno na Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa REA, Mhandisi Amos Maganga.
 Baadhi ya  Wafanyakazi na Menejimenti ya Wakala wa Nishati Vijijini (REA) wakiwa katika kikao chao na Waziri wa Nishati, Dkt Medard Kalemani kilichofanyika jijini Dodoma.
 Kamishna wa Umeme na Nishati Jadidifu, Mhandisi Leonard Masanja akiwasalimia Wafanyakazi na Menejimenti na Bodi ya Wakala wa Nishati Vijijini (REA) wakati wa kikao chao na Waziri wa Nishati, Dkt Medard Kalemani kilichofanyika jijini Dodoma. Kulia kwake ni Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa REA, Mhandisi Amos Maganga na kushoto kwake ni Mjumbe wa Bodi ya REA, Dkt Andrew Komba.
 Baadhi ya  Wafanyakazi na Menejimenti ya Wakala wa Nishati Vijijini (REA) wakiwa katika kikao chao na Waziri wa Nishati, Dkt Medard Kalemani kilichofanyika jijini Dodoma.
Kaimu Katibu Mkuu Wizara ya Nishati, Raphael Nombo, akizungumza na  Wafanyakazi, Menejimenti na Bodi ya Wakala wa Nishati Vijijini (REA) wakati wa kikao chao na Waziri wa Nishati, Dkt Medard Kalemani  (kushoto) kilichofanyika jijini Dodoma.